RSS
Kiongozi Muadhamu apanda miti katika Wiki ya Maliasili (2010/03/09 - 17:44)

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo amepanda miti miwili katika maadhimisho ya Wiki ya Maliasili. Shughuli hiyo imehudhuriwa pia na Waziri wa Jihadi ya Kilimo, Mkuu wa Shirika la Taifa la Kulinda Mazingira na Meya wa Jiji la Tehran.  

Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa kupanda miti ni kupandikiza nyenzo za uhai. Ameashiria kuwa miti na mimea ni dhihirisho la uhai na maisha na akasema: "Shughuli hii ya kupanda miti ni ishara ya kuwahimiza vijana watanashati na wananchi azizi hapa nchini juu ya umuhimu wa kupanda miti na kueneza ada hiyo nzuri."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo juu ya kulindwa utajiri mkubwa na wenye thamani wa taifa na akasema kuwa hatua ya kupanda miti hii leo ni somo la kutufunza thamani ya miti na iwapo tutapenda na kutumia vyema misitu ambao ni utajiri mkubwa wa kijadi hapa nchini, kamwe utajiri huo hautakwisha, kwani utajiri huo ni wa kimaumbile na unaojadidika.

Ayatullah Ali Khamenei amezitaka jumuiya na taasisi zinazohusika la suala la kulinda maliasili kuzuia utumia mbaya wa misitu na maliasili hususan zile zilizoko karibu na miji mikubwa.