Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran
Ayatullah Ali Khamenei leo amekutana na viongozi wa serikali na wananchi wa
matabaka mbalimbali kwa mnasaba wa kuadhimisha Maulidi ya Mtume wa nuru,
uadilifu na rehma Muhammad (saw) na mjukuu wake Imam Ja'far Swadiq (as).
Ayatullah Khamenei amesisitiza katika hadhara hiyo kwamba kuzalisha upya hakika
na maarifa ya Kiislamu na kutekeleza mafundisho ya Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi
Mungu ndiyo haja kubwa zaidi ya umma wa Kiislamu. Amesema kuwa umoja na
mshikamano wa wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu ndio wenzo wa kutatua
matatizo mbalimbali na sababu ya maendeleo na ustawi wa ulimwengu wa Kiislamu.
Katika hadhara hiyo ambayo imehudhuriwa pia na viongozi wa
ngazi za juu wa mfumo wa Kiislamu hapa nchini, mabalozi wa nchi za Kiislamu, wageni,
maulamaa na wanafikra wa Kiislamu walioshiriki kwenye Mkutano wa Kimataifa wa
Umoja wa Kiislamu uliomalizika leo mjini Tehran, Ayatullah Ali Khamenei amewapa
Waislamu wote mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa Maulidi na kuzaliwa
kiini cha matukufu yote ya Mwenyezi Mungu na Nabii Mteule Muhammad bin Abdullah
(saw) na wasii wake wa kweli, muenezaji wa Uislamu halisi Imam Ja'far Swadiq
(as) na akasema: "Matukufu yote ya kibinadamu na maadili mema yametokana
na kuzaliwa kutukufu kwa Mtume katika giza kubwa la ujinga, upotovu na
mghafala.
Amesema umma wa Kiislamu unahitajia mno kutafakati na
kusoma upya mafundisho na uongofu wa Mtume wa Mwisho (saw). Ameashiria jamii
kubwa ya umma wa Kiislamu, nafasi nzuri ya kijiografia, utajiri mkubwa, vipawa
na uwezo wa kibinadamu vya ulimwengu wa Kiislamu na akahoji kwamba, kwanini
ulimwengu wa Kiislamu ukawa katika hali ya mparaganyiko na kusumbuliwa na
matatizo mengi kama ufukara, ubaguzi, kubakia nyuma kielimu na udhaifu wa kiutamaduni
licha ya kuwa na sifa hizo adhimu, na wala hauwezi kutetea haki zake mbele ya
madhalimu wa ulimwengu?
Akibainisha udhaifu wa ulimwengu wa Kiislamu na kutoweza
kwake kutetea haki za Waislamu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametolea
mfano kadhia ya Palestina na akasema kughusubiwa ardhi ya kihistoria na
takatifu ya Palestina na dhulma isiyokuwa na kikomo na ya siku zote ya Wazayuni
watenda jinai dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Palestina ni jeraha kubwa linalousumbua
mno mwili wa umma wa Kiislamu; lakini ulimwengu wa Kiislamu unaamiliana na kadhia
hiyo kana kwamba suala la Palestina haliuhusu.
Ayatullah Ali Khamenei amelitaja dola bandia na la Kizayuni
la Israel kuwa ni donda hatari la saratani na akaongeza kuwa njia pekee ya
kujilinda mbele ya saratani hiyo angamizi na waungaji mkono wake ni kurejea
kwenye Uislamu na kuyapa umuhimu mafundisho ya Mtume Mtukufu wa dini hiyo.
Vilevile amefafanua sababu za kushindwa ulimwengu wa
Kiislamu katika kutetea haki za wafuasi wa dini hiyo akiashiria njama za mara
kwa mara za Marekani, Uingereza na maadui wengine wa Uislamu katika kuzusha
hitilafu na mfarakano katika umma na akasema: "Madhalimu hao mabeberu
wanaelewa vyema kwamba hitilafu na migawanyiko inaufanya umma wa Kiislamu uwe
mbali na kadhia muhimu mno ya Palestina, kwa sababu hiyo wanatumia kila
linalowezekana kuchochea moto wa mifarakano ya kikabila, kimadhehebu na
kijiografia katika nyoyo za Waislamu wa Shia na Suni na wafuasi wa madhehebu
nyingine za Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa haja
nyingine kubwa ya umma mkubwa wa Kiislamu ni kujenga upendo na umoja na ametoa
wito kwa serikali, wanafikra, maulamaa, wanahakati wa masuala ya kisiasa na
kijamii wa nchi za Kiislamu kutekeleza wajibu wao wa kuimarisha umoja na
mshikamano. Amesema iwapo mwamko wa Kiislamu utapanuka na kuimarika zaidi, na
nyoyo za Waislamu zikakurubiana zaidi na zaidi, njia ya kuamiliana, ushirikiano
na maendeleo ya Waislamu wote itafunguliwa na matatizo mengi ya ulimwengu wa
Kiislamu likiwemo suala la Palestina, yatapatiwa ufumbuzi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa madhehebu zote za Kiislamu
zinakubaliana kwamba ni wajibu kulinda na kutetea ardhi za Kiislamu
zinazoshambuliwa na kuvamiwa. Ameongeza kuwa hata hivyo na licha ya kuwa na
mtazamo wa aina moja kuhusu kadhia hiyo, inasikitisha kwamba ulimwengu wa
Kiislamu umeathiriwa na njama za Marekani na Uingereza za kuzusha mifarakano na
hitilafu kati ya Shia na Suni na madhehebu nyingine za Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema moja ya malengo
yanayopewa kipaumbele na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni umoja wa Waislamu na
kutetea kadhia ya Palestina. Amekumbusha maneno ya hayati Imam Ruhullah Khomeini
na sisitizo lake juu ya umoja na mshikamano wa Kiislamu na kadhia ya Palestina
na akasema: "Mfumo wa Kiislamu wa Iran, viongozi wote wa nchi na taifa
kubwa la Iran linayatambua masuala hayo ya kimsingi kuwa ni wajibu wake wa
kisheria na kidini na kauli na msimamo wao wote ni mmoja katika masuala
hayo."
Ameongeza kuwa mwamko unaoongezeka kila siku wa umma wa
Kiislamu na sauti za mataifa mbalimbali za kutetea Plestina ni mwangwi nzuri wa
misimamo ya haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika fikra za watu wa ulimwengu
wa Kiislamu. Ayatullah Khamenei amesema: "Nchi za Kiislamu pia zinapaswa
kumfuata Mtume Mtukufu kwa kuimarisha umoja wa Waislamu na kutetea haki zao
hususan katika kukabiliana na donda la saratani yaani Israel ghasibu na
waungaji mkono wake, ili umma wa Kiislamu uweze kufikia maendeleo na ufanisi wa
dunia na akhera kwa msaada wake Mola Muweza.
Mwanzoni mwa mkutano huo Rais Mahmoud Ahmadinejad wa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwapongeza Waislamu wote kwa mnasaba wa Maulidi
na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Mtume wa upendo na mahaba na mjumbe wa elimu
na hikima na akasema: "Jamii ya sasa ya mwanadamu inahitajia zaidi maarifa
na mfumo wa Mtume wa Mwisho Muhammad (saw) kuliko wakati wowote mwingine ili
kuweza kuangamiza ujahili na ubeberu, ukatili na kuwadunisha watu na hitilafu
na ubaguzi na hatimaye vipawa vya mwanadamu kote ulimwenguni vipate fursa ya
kuchanua kwa kusimamishwa uadilifu.
Dakta Ahmadinejad amezungumzia pia ujumbe unaompa mwanadamu
saada na ufanisi wa kuzaliwa Mtume wa Mwisho Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu
iwe juu yake na Ali zake na akaongeza kuwa baada ya ushindi wa Mapinduzi adhimu
ya Kiislamu, taifa la waumini la Iran lilishika bendera ya kupigania haki na
uadilifu na litaendeleza njia hiyo kwa umoja na mshikamano wa Waislamu.
Mwishoni mwa mkutano huo, maulamaa na wanafikra wa Kiislamu
walioshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu walifanya
mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika anga ya kirafiki na kidugu.