Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran leo amekutana na washiriki katika mkutano wa Mawaziri wa Viwanda wa nchi wanachama katika kundi ya D8 uliomalizika leo mjini Tehran. Ayatullah Ali Khamenei ameashiria masuala ya kiutamaduni na Kiislamu yanayozikutanisha pamoja nchi hizo, nafasi yao nyeti mno ya kijiografia katika mabara ya Asia na Afrika, jamii inayozidi watu bilioni moja na utajiri wa maliasili ya nishati na akasema: "Ushirikiano wa nchi hizo nane za unaweza kuwa kigezo cha kuigwa na nchi zote za Kiislamu. Amesisitiza kuwa kudumishwa ushirikiano wa kiviwanda kati ya nchi hizo kutakuwa na taathira chanya kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia uungaji mkono na himaya ya Iran kwa ushirikiano wa nchi za Kiislamu tangu mwanzoni mwa kuanzishwa kundi la D8 na akasema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa mafanikio yake ya kisayansi na kiviwanda kwa nchi za Kiislamu.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria pia tabia ya nchi za kibeberu ya kutumia elimu na sayansi kwa ajili ya kuzidhibiti nchi nyingine na akasema: "Nchi za Kiislamu zinapaswa kutumia uwezo wao mkubwa wa nguvu ya kazi ya kibinadamu, utajiri wa maliasili, vipawa vikubwa na ushirikiano baina yao na kuzifikisha nchi zao katika nafasi inayostahiki.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kutekelezwa makubaliano ya mkutano wa Tehran na akasema nchi nane wanachama wa D8 zinapaswa kufanya bidii ya kutekeleza kimatendo makubaliano hayo na kupiga hatua katika njia ya kuzidisha ushirikiano na maendeleo ya kiviwanda kwa imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu.
Mwanzoni mwa mkutano huo Waziri wa Viwanda wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ali Akbar Mehrabian amesema kuwa mkutano wa sasa ambao ni kwanza wa Mawaziri wa Viwanda wa kundi la D8 umefanyika kwa ubunifu wa Iran, suala ambalo lina umuhimu mkubwa katika ushirikiano wa nchi wanachama.
Bwana Mehrabian amesema kuwa taarifa ya mwisho ya mkutano huo wa Tehran itakuwa ramani ya njia ya ushirikiano wa kiviwanda wa nchi hizo na kwamba imepasishwa na nchi zote nane za D8.
Waziri wa Viwanda wa Uturuki Nihat Argon pia amesema kuwa kufanyika mkutano huo mjini Tehran kumekuwa na mafanikio makubwa na akaongeza kuwa ana matarajio mikutano hiyo itaimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kijamii wa nchi wanachama.
Waziri wa Viwanda wa Uturuki amesema mawaziri hao wameazimia kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika nchi zao na kutayarisha mazingira mazuri ya shughuli za wawekezaji na wamiliki wa viwanda.
Waziri wa Viwanda wa Bangladesh pia amehutubia kikao hicho akisema kuwa mkutano wa Mawaziri wa Viwanda wa kundi la D8 mjini Tehran ni mwanzo mzuri kwa ajili ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama na kuboresha sekta ya viwanda na teknolojia ya nchi hizo. Amesema kuwa taarifa ya mwisho ya mkutano wa Tehran ni waraka mzuri kwa ajili ya ushirikiano.
Ameongeza kuwa mgogoro wa sasa wa kiuchumi duniani hauwezi kutatuliwa kirahisi, kwa msingi huo nchi wanachama wa kundi la D8 zinapaswa kushirikiana zaidi katika nyanja zote.