RSS
Wajibu mkubwa zaidi wa mabalozi wa utamaduni wa Iran ni kuonesha taswira sahihi ya Mapinduzi ya Kiislamu (2010/03/02 - 17:17)

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mapema leo amehutubia hadhara iliyowakutanisha pamoja Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu, Mkuu wa Jumuiya ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu na wawakilishi wa masuala ya utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi akisisitiza kuwa nguvu halisi ya nchi hii ni nguvu na kiutamaduni. Ayatullah Khamenei amesema moja ya majukumu mazito ya mabalozi wa utamaduni wa utawala wa Kiislamu nje ya nchi ni kuonesha taswira sahihi na halisi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ukweli wa mambo na maendeleo ya Iran ya sasa sambamba na kueneza lugha na fasihi ya Kifarsi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria nafasi na umuhimu mkubwa wa shughuli na mawasiliano ya kiutamaduni na akasema: "iwapo kazi za kiutamaduni zitafanyika kwa njia sahihi na kuathiri fikra na nyoyo za watu, hapana shaka kwamba zitajaza nafasi ya wazi ambayo yumkini ikajitokeza katika medani ya udiplomasia au katika uhusiano wa kibiashara na kiuchumi.

Ayatullah Khamenei amezungumzia pia mbinu za nchi za kikoloni kwa ajili ya kutimiza malengo yao ya kidhalimu kwa kutumia uhusiano na ushawishi wa kiutamaduni na akasema nchi hizo zinaendeleza malengo yasiyokuwa ya kibinadamu kwa kutumia harakati za kiutamaduni ilhali katika utawala wa Kiislamu ambao umeasisiwa kwa msingi wa haki na fikra zafi za mafundisho ya dini ya Mwenyezi Mungu, kunapaswa kutumiwa mbinu na nyenzo za kiutamaduni kwa njia bora na zinazofaa.

Amesema kuwa kutengwa halisi ni kutengwa kiutamaduni na akaongeza kuwa iwapo kazi za kiutamaduni zitafanyika kwa njia sahihi hakuna jambo lolote linaloweza kuitenga Iran.

Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya umuhimu na nafasi ya shughuli za kiutamaduni za mabalozi wa utamaduni wa Iran na akaongeza kuwa: "Mabalozi wa utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio mshtari wa mbele wa mpambano wa kiutamaduni katika medani ya kimataifa, na Jumuiya ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu ndiyo makao makuu ya mapambano hayo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua wajibu na majukumu mazito ya mabalozi wa utamaduni wa Iran akisema: "Moja ya makumu muhimu na kazi kubwa za mabalozi hao ni kutoa taswira sahihi ya Mapinduzi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa walimwengu na viongozi wa nchi mbalimbali.

Ayatullah Khamenei amezungumzia pia njama kubwa za kipropaganda za kambi ya ubeberu za kutaka kuonesha taswira mbaya kuhusu mfumo wa Kiislamu wa Iran na akasema kambi hiyo inataka kuwafanya walimwengu na wapenzi wa Iran wauchukie mfumo wa Kiislamu na kupunguza taathira ya kiroho na kimaanawi ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa kutoa taswira iliyotiwa dosari kuhusu mfumo wa Kiisalmu hapa nchini; kwa msingi huo wajibu muhimu zaidi wa wawakilishi wa masuala ya utamaduni wa Iran ni kutoa taswira sahihi kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Ali khamenei amesema sharti la kutoa taswira sahihi kuhusu mfumo wa Kiislamu ni kuuarifisha Uislamu kwa njia sahihi. Amesisitiza kuwa mabeberu na wasioitakia kheri Iran wanafanya jitihada za kuwalingania walimwengu Uislamu ambao ama ni wenye mitazamo finyu au Uislamu wa kiliberali usiokuwa na taathira. Amesisitiza kuwa Uislamu wa kweli na halisi unaokusudiwa na utawala wa Kiislamu hapa nchini una maana aali, za kina na za wazi kuhusu mwanadamu, Mwenyezi Mungu, ulimwengu wa baadaye na mahitaji ya kimaada na kiroho ya mwanadamu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa jukumu jingine la mabalozi wa utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuarifisha maendeleo makubwa ya kisayansi ya Iran, fasihi na sanaa ya nchi hii. Amesema kuwa majukumu mengine ya wawakilishi wa masuala ya utamaduni wa Iran ni kutangaza vielelezo vya demokrasia ya hapa nchini, mikusanyiko adhimu ya wananchi na madhihirisho ya kidini. Ameongeza kuwa mahudhurio ya kimaanawi ya matabaka mbalimbali ya wananchi hususan vijana katika shughuli za kidini kama majlisi za visomo vya Qur'ani, dua na majlisi za maombolezo ya kuwakumbuka watu adhimu ni mambo muhimu ambayo yanapaswa kudhihirishwa kwa walimwengu kwa kutumia njia za kisanii na filamu za matukio ya kweli.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kuarifishwa Iran ya sasa. Ametilia mkazo umuhimu wa lugha na fasihi ya lugha ya Kifarsi na akasema: "Moja ya kazi kuu za mabalozi wa utamaduni ni kueneza lugha ya Kifarsi kupitia njia ya kuanzisha mafunzo ya lugha hiyo katika vituo vya elimu na vyuo vikuu.

Ayatullah Khamenei ameishukuru pia Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu kwa kazi zake nzuri.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiisalmu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Muhammad Hussaini ametoa hotuba fupi akisema kuwa miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na ofisi za wawakilishi wa masuala ya kiutamaduni wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran nje ya nchi ni kupanua zaidi lugha ya Kifarsi, kuonesha shughuli mbalimbali za Iran, kufanya maonyesho ya masuala ya kiutamaduni na kisanii na makongamano ya kiutamaduni ya mara kwa mara.

Mkuu wa Jumuiya ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiisalmu ya Iran Bwana Mustafavi pia amehutubia mkutano huo akitoa ripoti kuhusu kikao cha nane cha wakuu wa vituo vya utamaduni vya Iran nje ya nchi.